Tarehe 10 Februari 2026, Mkurugenzi wa Taasisi ya Anjita Foundation, Bi. Janeth Christian Malela, alifanya mkutano wa kwanza na wataalamu wa ngazi ya serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.
Mkutano huo uliwakutanisha wataalamu kutoka Kitengo cha Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii pamoja na Ofisi ya Mhandisi wa Halmashauri. Lengo kuu la mkutano lilikuwa ni kuwasilisha mpango kazi na bajeti ya utekelezaji wa Mradi wa Malezi Center, unaofadhiliwa na Taasisi ya Tanzania ECD Network.
Mradi wa Malezi Center unalenga kujenga vituo vya kijamii vya kulelea watoto wadogo mchana katika Halmashauri za Wilaya ya Chalinze na Mkuranga. Kupitia mradi huu, ANJITA inalenga kuimarisha huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika jamii, ili kuhakikisha watoto wanapata msingi imara wa ukuaji wao.
Taasisi ya ANJITA inaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakuwa na tija kwa watoto, familia na jamii kwa ujumla.
