Anjita foundation kwakushirikiana na taasisi ya Visima Viwili Child and Youth Foundation na wanachama wa Tanzania ECD Network Mkoa wa Pwani, ilifanikiwa kuendesha hafla fupi ya ugawaji wa vifaa vya shule kwa watoto 288 wanaotoka katika mazingira magumu.
Watoto hao wanasoma kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita, na wanatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Bagamoyo, mkoa wa Pwani.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mheshimiwa Seif Wenge, Diwani wa Kata ya Mtongani – Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha. Katika hotuba yake, Mheshimiwa Wenge aliwahimiza watoto kuzingatia elimu, kuwa na uwajibikaji na kuzingatia nidhamu bora kama msingi wa kufanikisha ndoto zao za maisha.
Aidha, aliwakumbusha wazazi na walezi kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria, na kwamba jukumu la msingi la mzazi na mlezi ni kuwalinda watoto na kuhakikisha wanapata haki zao zote za msingi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Visima Viwili Child and Youth Foundation, Ndg. George Myinga, aliwashukuru wadau wote kwa moyo wao wa kujitolea na kwa mchango wao wa vifaa mbalimbali vya shule. Alitoa wito wa kuendeleza ushirikiano huo ili kufikia watoto wengi zaidi wenye uhitaji katika Mkoa wa Pwani na kwingineko.
Ndg. Myinga alisisitiza dhamira ya dhati ya taasisi ya Visima Viwili katika kuleta mabadiliko chanya na maendeleo endelevu kwa watoto na vijana, kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Akiwakilisha wanachama wa TECDEN mkoa wa Pwani, Bi. Janeth Christian Malela, ambaye ni Mkurugenzi wa Anjita Child Development Foundation, aliishukuru serikali, wazazi, walezi, wajasiriamali, viongozi wa dini, wafanyabiashara, taasisi na wadau wote kwa upendo na mshikamano waliouonesha kwa kuchangia vifaa hivyo.
Bi. Malela alisisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kuwaunga mkono watoto wanaoishi katika mazingira magumu, pamoja na kutoa malezi na makuzi chanya kwa watoto wetu kama msingi wa kujenga jamii bora na yenye maendeleo endelevu.






