Taasisi ya Anjita Child Development Foundation kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mkuranga wamefanya kikao cha tathmini ya mapitio ya utekelezaji wa shughuli za Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT–MMMAM) tarehe 11.2.2026.
Kikao hicho kililenga kutathmini hatua zilizofikiwa katika kuimarisha huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, hususani katika maeneo ya ulinzi na usalama wa mtoto, afya, lishe, malezi yenye mwitikio pamoja na fursa za ujifunzaji wa awali katika jamii.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Happiness Kikowe, aliwasilisha matumizi ya ECD Score Card inayotumika kufuatilia na kupima utekelezaji wa shughuli za MMMAM.
Bi. Happiness alieleza namna ya ujazaji sahihi wa taarifa, ukusanyaji wa takwimu muhimu na taratibu za uwasilishaji wa taarifa kupitia mfumo wa score card, akisisitiza umuhimu wa takwimu sahihi katika kupanga na kuboresha huduma za watoto.
Katika uwasilishaji wa taarifa ya robo ( Oktoba hadi Disemba, 2025), mafanikio yaliyobainishwa ni pamoja na:
Kutoa elimu kwa vituo 56 vya DCC kuhusu kuelimisha wazazi/walezi wenye watoto wa miaka 5 kuwasajili darasa la awali, kuimarisha uelewa wa jamii juu ya masuala ya malezi na makuzi ya watoto ngazi ya kaya na jamii.
Aidha, Bi. Happiness aliwakumbusha na kuwasisitiza washiriki kuendelea kuelimisha jamii pamoja na Wakuu wa Vitengo/ idara kuona namna ya kuwezesha/ kusaidia shughuli zaa Malezi na Makuzi kupitia shughuli wanazozitekeleza kila siku, akisisitiza kuwa suala la malezi ni la mtambuka na linahitaji ushirikiano wa sekta zote.
Nae Afisa Maendeleo ya jamii, alisisitiza kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya Malezi, Makuzi na Maendeleo yao ya awali.
Katika kikao hicho , Afisa Ustawi wa jamii aliwasilisha tena mradi wa Malezi center unaofadhiliwa na TECDEN wenye kulenga kujenga kituo 1 cha kijamii cha kulelea watoto wadogo mchana kinatarajiwa jengwa katika kata ya mkuranga wilayani humo.



